top of page

Safari ya Uhai

Public·45 members

USIKU NDIO UKWELI HUTOKA – SIKILIZA MOYO WAKO


Kuna kitu cha ajabu sana kuhusu usiku ambacho wengi hawakielewi. Mchana unaweza kujaza kelele, shughuli, watu, na vicheko vya kujilazimisha… lakini usiku ukifika, kila kitu kinatulia. Hakuna distraction. Hakuna kujificha. Ni wewe na nafsi yako tu. Na hapo ndipo ukweli huanza kuongea. Nina kumbuka kuna kipindi nilikuwa nakimbia sana hisia zangu. Nilijaza siku zangu na shughuli, nikawa bize kupita kiasi, si kwa sababu nilikuwa na kazi nyingi sana… bali kwa sababu nilikuwa naogopa kukaa kimya. Kwa sababu nilijua nikikaa kimya, kuna sauti itanifuata. Sauti ambayo haipigi kelele, lakini ina nguvu kuliko zote.


Usiku ulipofika, mambo yalibadilika. Nili lala kitandani, taa zime zimwa, simu pembeni… halafu ghafla mawazo yanaanza kuja. Sio yale ya kawaida. Ni yale unayo yakimbia mchana. Kumbukumbu, maamuzi, watu, makosa… kila kitu kina jitokeza bila ruhusa. Na hapo ndipo nilipo anza kuelewa usiku hauleti mawazo mapya, una funua yale uliyokuwa una yaficha.

Sasa nikuulize… Je, umewahi kujikuta usiku unawaza kitu ambacho mchana ulikipuuza?Je, umewahi kuhisi kama moyo wako una kuambia kitu fulani, lakini una kipotezea kwa sababu hakikufurahishi? Huo ndio ukweli. Moyo hauongei kwa kelele. Haukulazimishi. Unakupa ishara ndogo ndogo. Lakini kwa sababu mchana tuna kelele nyingi watu, kazi, mitandao, majukumu hatuusikii. Mpaka usiku unapokuja na kutuliza kila kitu, ndipo ile sauti ndogo inakuwa wazi.

Na mara nyingi, hiyo sauti huwa sahihi. Lakini watu wengi wana ikwepa. Kwa sababu ukweli si rahisi kuupokea. Ni rahisi kujidanganya kwamba uko sawa, kwamba unafuraha, kwamba umechagua vizuri… kuliko kukubali kwamba kuna kitu ndani hakiko sawa. Ndiyo maana baadhi ya watu wanaogopa hata kulala bila kelele lazima kuwe na muziki, TV, au simu. Wanatafuta kitu cha kuzima ile sauti ya ndani. Lakini ukweli unabaki pale pale. Nilikuja kugundua kwamba kila nilipo puuzia ile sauti ya usiku, nilijikuta nikifanya maamuzi mabaya mchana. Nilikuwa najiaminisha mambo ambayo si ya kweli. Lakini kila nilipo amua kuisikiliza, hata kama inaumiza, ilinisaidia kuona mambo kwa uwazi zaidi.


Usiku unakuuliza maswali ambayo hakuna mtu mwingine atakuuliza. Je, kweli una furaha au unajifanya? Je, watu ulio wazunguka wana kujenga au wana kumaliza pole pole? Je, njia uliyo chagua ni yako… au ni ya kuwafurahisha wengine? Na majibu yako, yako ndani yako tayari. Tatizo ni kwamba wengi wetu hatutaki kuyasikia. Lakini kuna nguvu kubwa sana kwenye kukubali ukweli wako mwenyewe. Ndiyo mwanzo wa mabadiliko halisi. Ndiyo mwanzo wa kujijua. Ndiyo mwanzo wa kuishi maisha ambayo si ya maigizo. Kwa hiyo leo usiku, kabla hujalala…


  • Usikimbie.


  • Usijifiche.


  • Usizime ile sauti.


  • lSikiliza.


Kwa sababu wakati dunia imelala, ndipo nafsi yako inaamka na kusema ukweli wote ambao umekuwa ukikwepa. Na swali la mwisho ni hili… Uko tayari kuusikia ukweli wako… au bado unahitaji kelele za mchana ili ujifiche?


#YusufMgunya

#SafariYaUhai

2 Views
bottom of page